Kenya yapata ruzuku ya shilingi 59.7B kutoka kwa Global Fund

Martin Mwanje
3 Min Read

Kenya imepokea ruzuku yenye thamani ya shilingi bilioni 59.7 ambazo ni sawa na dola milioni 407,989,068 za Marekani kutoka kwa Global Fund kusaidia mapambano dhidi ya magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

Ruzuku hiyo, ambayo itatolewa kuanzia Julai, 2024 hadi Juni 2027, inalenga kusaidia kuimarisha mifumo ya afya na jamii kote nchini.

Fedha hizo zinajumuisha dola 232,580,654 kwa ajili ya kupambana na Ukimwi, dola 72,934,665 kupambana na Malaria na Ddola 67,785,529 za kukabiliana na Kifua Kikuu.

Dola 34,688,220 zitatumiwa kuimarisha mifumo ya afya nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, Global Fund ni ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi, na watu walioathiriwa na magonjwa yanayolenga kuongeza kasi ya kukomesha UKIMWI, Kifua Kikuu, na milipuko ya Malaria duniani.

Tangu kuanzishwa mwaka 2003, Global Fund imekuwa ikisaidia katika ununuzi wa bidhaa kama vile dawa za kurefusha maisha (ARVs), vifaa vya kupima Ukimwi, kondomu, na vitendanishi vya maabara, na pia imechangia katika uingiliaji wa programu katika vituo vya afya na ngazi ya jamii.

Aidha, imebainika kuwa Kenya imeshuhudia kupungua kwa viashiria vinavyohusiana na Ukimwi: maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 78, vifo vinavyotokana na Ukimwi kwa asilimia 68 na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa asilimia 65.

“Upungufu huu mkubwa unatokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za upimaji wa Ukimwi, matibabu na kinga katika ngazi ya jamii na kituo. Kwa sasa, takriban watu milioni 1.4 wanaoishi na virusi wanapokea matibabu katika vituo mbalimbali nchini kote nchini,” ilisema taarifa ya Wizara ya Afya.

Wizara ya afya ilihusisha maendeleo hayo na ugatuaji wa huduma za Ukimwi na ushirikiano kati ya serikali, washirika wa maendeleo, watendaji wasio wa serikali, wadau, kaunti na jamii.

Zaidi ya hayo, kiwango cha mafanikio ya matibabu ya Kifua Kikuu kimeongezeka hadi asilimia 86 na wastani wa kiwango cha chanya kati ya wagonjwa wa TB umeshuka kutoka asilimia 7.35 mwaka 2021 hadi asilimia 5.6 Machi, 2024. Idadi ya watu waliopimwa TB iliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka 245,902 mwaka 2021 hadi 502,970 Machi, 2024.

Katika vita dhidi ya Malaria, maambukizi ya kitaifa yamepungua kutoka asilimia 8.2 mwaka 2015 hadi asilimia 6 mwaka 2023.

Global Fund pia umeshirikiana na serikali na kutoa msaada kwa ajili ya uanzishwaji wa vitengo vya afya ya jamii 1,933, mafunzo ya wahamasishaji wa afya ya jamii 18,500.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *