Serikali inalenga kuzalisha majani chai yaliyoongezwa thamani, huku ikiweka mkakati wa miaka mitano wa kupanua masoko, ikilenga masoko 13 mapya ughaibuni.
Waziri wa kilimo na ustawi wa mifugo Mithika Linturi, amesema ili kuimarisha ushindani wa majani chai kutoka Kenya, serikali imekumbatia uongezaji thamani pamoja na kubuni aina mbali mbali za majani chai, kuwiana na mpango wa serikali wa kuimarisha uchumi wa Bottom Up(BETA).
“Chini ya uongozi wa Rais William Ruto, tumeanzisha ushirikiano wa kimataifa ili kupeleka mbele sekta ya majani chai nchini,” alisema waziri Linturi.
Waziri Linturi aliyasema hao leo Jumanne wakati wa kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Majani Chai, iliyoandaliwa katika kaunti ya Nandi.
Aidha waziri huyo alipongeza ufanisi ambao umeshuhudiwa katika sekta ya majani chai nchini, ambapo taifa hili lilipata shilingi bilioni 196 kutokana na mauzo ya majani chai mwaka jana.
Kulingana na waziri huyo, shilingi bilioni 180 zilipatikana kutokana na mauzo ya nje ya nchini, huku shilingi bilioni 16 zikipatikana kutokana na mauzo ya hapa nchini.
Alisema ufanisi huo ni kutokana na juhudi za serikali za kufanya mageuzi katika sekta hiyo ya majani chai.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa dijitali Eliud Owalo, naibu gavana wa Nandi Dkt. Yulita Chebotip, naibu kamishna wa kaunti hiyo, wadau wa majani chai na wakulima wa zao hilo miongoni mwa wengine.