Kenya imetoa wito wa ushirikiano thabiti kati ya Afrika na Korea Kusini ili kufanikisha ukuaji endelevu na ushughulikiaji wa pamoja wa changamoto ibuka duniani.
Akizungumza kwenye mkutano wa Mawaziri wa Afrika na Korea Kusini Jijini Seoul, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alidokeza kuwa ushirikiano ulioimarishwa kati ya Afrika na Korea Kusini, ni muhimu katika kuchochea ubadilishanaji wa teknolojia, maarifa na ukuaji wa viwanda.
Mudavadi aliangazia majukumu ya taasisi kama vile Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) na Benki ya Korea ya Exim, katika kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi ya Kenya, ubadilishanji wa teknolojia na ukuaji wa sekta ya kibinafsi.
“Afrika na Korea Kusini lazima ziimarishe ushirikiano ambao unainua ufanisi wa pamoja, ukuaji endelevu na ushughulikiaji wa pamoja wa changamoto ibuka duniani,” alisema Mudavadi.
Aliyasema hayo alipowakilisha mipango ya maendeleo ya Kenya kwenye mkutano huo, huku akidokeza kuwa kuendelea kwa Korea Kusini kuwekeza katika miradi kama vile Konza Technopolis na taasisi iliyozinduliwa hivi karibuni ya Sayansi na Teknolojia (Kenya-AIST), kunaashiria kuimarika kwa ushirikiano katika ya Kenya na Korea Kusini katika masuala ya teknolojia, uvumbuzi na viwanda.
“Ushirikiano huu unaiweka Kenya kuwa kitovu cha uongezaji thamani, uvumbuzi na ukuaji endelevu wa uchumi katika kanda hii,” aliongeza Mudavadi.