Serikali ya Kenya na ile ya Hungary, zimetia saini Mikataba miwili ya Maelewano kuhusu Elimu na Kilimo, huku zikinuia kuimarisha uhusiano na kubuni fursa zaidi za ushirikiano na ukuaji.
Kupitia mtandao wa X, Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, alisema taifa la Hungary linasalia kuwa mshirika mkuu wa Kenya hasaa katika sekta ya Elimu, huku ikitoa nafasi 200 kwa wanafunzi wa Kenya kusomea huko kila mwaka.
“Mpango huu huimarisha uhusiano baina ya watu na huleta mageuzi katika chumi za nchi hizi.” alisema Mudavadi.
Mkataba huo katika sekta ya Elimu unalenga kuimarisha ushirikiano katika Elimu ya juu, vyuo vya kiufundi na utafiti baina ya nchi hizo mbili.
Katika sekta ya Kilimo, nchi hizo mbili zilikubaliana kushirikiana katika utaalam na mbinu bora za kuongeza uzalishaji wa mazao, biashara ya mazao ya kilimo na ubadilishanaji teknolojia.
“Mikataba hiyo ya Maelewano ni ishara ya hatua za kukuza ushirikiano na ukuaji baina ya nchi hizi mbili,” alisema Mudavadi.