Kenya inapania kutuma ombi la kuandaa msururu mmoja wa mashindano ya raga ulimwenguni mwaka 2027 na pia mashindano ya Afrika kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2026.
Kulingana na Mwenyekiti wa chama cha raga nchini Kenya KRU Sasha Mutai, tayari wamefanya vikao kadhaa na maafisa wakuu wa shirikisho la raga duniani wakati wa fainali za kombe la dunia maajuzi nchini Ufaransa.
Kenya ilishushwa ngazi kutoka kwa mashindano ya msururu wa dunia msimu uliopita na watalazimika kushiriki mashindano Challenger kuanzia Januari mwaka ujao, ili kuwania nafasi ya kurejeshwa.
Wakati uo huo mabadiliko matano yamefanyiwa kikosi cha timu ya Kenya kwa wachezaji 15 upande, kitakachoshiriki mchuano wa marudio ya kombe la Elgon dhidi ya Uganda siku ya Jumamosi katika uwanja wa Jomo Kenyatta International Stadium huko Mamboleo kaunti ya Kisumu.
Eugene Sifuna atarejea kikosini baada ya kukosa duru ya kwanza wakishirikiana na Ephraim Oduor na Hillary Mwanjilwa wanaotwaa nafasi za Wilhite Mususi na Teddy Akala, waliocheza mkumbo wa kwanza wiki iliyopita ambapo Kenya ilishindwa pointi 20-21 na Uganda jijini Kampala.
Wanandinga watakaokosa mechi hiyo ni pamoja na Emmanuel Otieno, Reinhard Mwalati na Walter Okoth huku Andrew Matoka akijumuishwa kikoisni ilihali Shem Okola amejumuishwa timuni kwa mara ya kwanza.