KeNHA yafunga barabara ya Mai Mahiu-Narok kutokana na mafuriko

Dismas Otuke
1 Min Read

Mamlaka ya kitaifa ya barabara kuu nchini KENHA,imefunga barabara kuu ya Mai Mahiu -Suswa-Narok, kufuatia kuharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Kulingana na KeNHA ,hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia vifusi vya maporomoko ya ardhi vilivyojaa barabarani baada ya kusombwa na maji ya mafuriko.

Kwenye taarifa ya Jumatatu jioni  KeNHA, imefunga barabara hiyo ili kuondoa vifusi kwenye barabara hiyo ya umbali wa kilomita 27 kutoka mji wa Mahi Mahiu hadi mjini Narok.

Wasafiri wa magari wameshauriwa kutumia barabara mbadala ikiwemo  barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Zaidi ya watu 50 wanakisiwa kuaga dunia kufuatia mkasa wa kupasuka kwa bwawa kijijini Kiandama eneo la Mai Mahiu, ambapo nyumba zilisombwa na maji ya mafuriko huku wengine zaidi ya 100 wakipokea matibabu hospitalini.

Takriban watu 166 wameripotiwa kufariki kote nchini kutokana na mafuriko kwa mjibu wa msemaji wa serikali Isaack Mwaura.

Share This Article