Siku chache baada ya baraza la maaskofu wa kanisa katoliki kulalama kuwa hospitali zinazomilikiwa na mashirika ya kidini zinaidai iliyokuwa hazina ya taifa ya matibabu NHIF, serikali imeahidi kulipa deni hilo hivi karibuni.
Kupitia kwa taarifa, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema serikali katika muda wa siku chache zijazo itatoa kitita cha shilingi bilioni 2.5, ili kulipa deni linalodaiwa NHIF.
Kulingana na Mwaura, serikali tayari imetoa shilingi milioni 938 za kulipa deni hilo ambalo NHIF inadaiwa na vituo vya afya nchini, vikiwemo vile vinavyomilikiwa na mashirika ya kijamii.
“Serikali inatoa hakikisho kwamba, madeni yote yatalipwa ili kutoa fursa kwa vituo vya afya kuendelea kuwahudumia wakenya kikamilifu,” alisema Mwajra kupitia taarifa.
Hatibu huyo wa serikali alisema hadi kufikia sasa, wakenya milioni 14, wamejisajili kwa hazina ya afya ya jamii SHIF.
Viongozi hao wa kanisa katoliki, waliishutumu serikali kwa kukosa kulipa deni la shilingi milioni tatu, ambalo iliyokuwa NHIF inadaiwa na vituo vya afya vinayomilikiwa na mashirika ya kidini.