Kanja: Kuingia uwanja wa ndege bila ruhusa haikubaliki

Martin Mwanje
2 Min Read

Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja ameonya kuwa serikali haitakubali mtu yeyote kuingia katika uwanja wa ndege bila kibali. 

Aidha, Kanja ameongeza kuwa kuingia katika maeneo yanayolindwa bila ruhusa ni jambo lisiloweza kuvumilika.

Vijana wa Gen Z wametishia kuingia katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA leo Jumanne, katika hatua ambayo inahofiwa itakuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Hatua hiyo pia inahofiwa kwamba itatatiza kwa kiwango kikubwa usafiri wa ndege uwanjani hapo.

“Ile mambo ambayo inaendelea kwa yetu saa hizi si mambo sawasawa na hatutakubalia. Kwenda kuingia kwa kiwanja ya ndege huko na hujapata ruhusa ya kuingia huko haitakubalika,” alionya Kanja wakati akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi leo Jumanne asubuhi.

“Nataka kukumbusha Wakenya wote, hatuna nchi nyingine inaitwa Kenya, ni hii peke yake tuko naye. Na sisi wote tuko na jukumu la kuona ya kwamba nchi yetu iko sawasawa na iko na amani ya kutosha.”

Kanja aliyewahutubia wanahabari akiwa ameandamana na maafisa wengine wa usalama akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Amin Mohamed, badala yake amewaomba Wakenya kuwajibika na kuilinda nchi hii akionya kuwa ikiwa itasambaratika, hakuna mahali pengine ambako watakimbilia.

Usalama katika uwanja wa JKIA, sawia na maeneo mengine yanayolindwa kisheria kama vile majengo ya bunge umeimarishwa wakati vijana hao wakitarajiwa kujitosa mitaani kuendelea na maandamano yao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *