Kamati ya bunge kuhusu mshikamano yafanya mkutano na NCIC huko Mombasa

Marion Bosire
2 Min Read
Liza Chelule, Naibu Mwenyekiti kamati ya mshikamano na fursa sawa bungeni

Naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu mshikamano na fursa sawa Liza Chelule, leo aliongoza mkutano kati ya kamati hiyo na tume ya ushirikiano na mshikamano wa kitaifa NCIC huko Mombasa.

Kikao hicho kiliangazia yaliyomo kwenye ripoti ya kamati ya kitaifa ya mazungumzo NADCO na kusisitiza jukumu la NCIC katika kuimarisha fursa sawa na amani kati ya wakenya.

Kamati ya mshikamano ya bunge iliongoza majadiliano kuhusu ripoti ya NADCO inayoangazia ukosefu wa usawa katika fursa serikalini.

Ripoti hiyo inalenga kukuza ujumuishaji na maelewano kati ya jamii tofauti nchini Kenya, kufungamana na jukumu la kikatiba la kamati hiyo ya bunge na NCIC.

“Tumepatiwa jukumu la kuhakikisha kwamba sheria zinazopendelea mshikamano na fursa sawa hazipendekezwi tu lakini pia zinatekelezwa ipasavyo na mashirika husika.” alisema Chelule.

Mbunge huyo wa kaunti ya Nakuru alitambua juhudi zinazoendelea za kamati hiyo ya bunge na NCIC za kuendeleza mchakato mzima.

Chelule alipongeza wanachama wa kamati ya bunge kuhusu mshikamano na fursa sawa kwa kumuunga mkono tangu alipoteuliwa kuwa naibu mwenyekiti chini ya uongozi wa Adan Haji, mbunge wa Mandera.

Alisema mkutano wa leo ni hatua muhimu katika kuboresha ushirikiano kati ya bunge na NCIC kuhakikisha sera zinazohimiza umoja wa kitaifa na mshikamano zinapatiwa kipaumbele na kuafikiwa kote nchini.

Wahusika wa mkutano huo walithibitisha kujitolea kwao kwa kanuni za usawa na mshikamano wakitambua majukumu yao katika kuunda wakati ujao wenye usawa kwa wakenya wote.

Website |  + posts
Share This Article