Kamati ya bunge kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mambo ya Nje, inalenga kuwashirikisha washikadau katika juhudi zake za kuendeleza uchunguzi kuhusu operesheni za wanajeshi wa Uingereza wanaofanya mazoezi hapa nchini (BATUK).
Ikiongozwa na naibu mwenyekiti wake Meja Mstaafu Bashir Abdullahi, kamati hiyo ilikutana ili kupanga mikakati ya kutekeleza uchunguzi huo.
Kamati hiyo itashauriana na mashirika ya kijamii na viongozi wa kidini katika kaunti zilizoathiriwa za Laikipia, Samburu na Isiolo.
Wawakilishi kutoka serikali ya kaunti ya Laikipia, Wizara ya Ardhi, afisi ya kiongozi wa mashtaka na wale wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, pia watafika mbele ya kamati hiyo kuhusu mienendo ya wanajeshi wa BATUK.
Aidha, kamati hiyo pia itafanya ziara za ukaguzi kuambatana na majukumu yake.
Wanachama wa kamati hiyo pia watachukua jukumu la kutathmimi utekelezaji wa bajeti kwa mashirika yaliyo chini ya BATUK kwa mwaka wa kifedha wa mwaka 2023/2024.