Jamaa na marafiki wa marehemu John Okafor mwigizaji wa filamu za Nollywood wametoa taarifa ya kuomba msaada wa kifedha kwa ajili ya mazishi yake miezi kadhaa baada ya kifo chake.
Kulingana na taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na viongozi kadhaa wa kamati ya mazishi akiwemo rais wa chama cha waigizaji nchini Nigeria Emeka Rollas, mazishi ni hafla ya siku tano na hivyo fedha nyingi zinahitajika.
Kutokana na hilo, kamati hiyo imefungua ukurasa katika jukwaa la mitandaoni la kuchangisha pesa kwa jina “Go Fund Me”.
Kuhusu pesa zilizochangishwa awali wakati alikuwa akiugua, kamati hiyo ilielezea kwamba zote zilitumika kugharamia matibabu yake ukiwemo upasuaji aliofanyiwa mara mbili.
Familia ya marehemu mwigizaji huyo ambaye wengi walimfahamu kama Mr. Ibu, awali ilitangaza Juni 28, 2024 kuwa tarehe ya mazishi ya mpendwa wao.
Ibu alifariki kutokana na mshtuko wa moyo Machi 2, 2023 katika hospitali ya Evercare jijini Lagos baada ya kulazwa kwa muda mrefu ambapo alikatwa mguu mmoja.