Jaji Mkuu Martha Koome ametoa wito kwa maafisa wa polisi kufanya kila wawezalo kuepuka kusababisha maafa wakati wa maandamano ambayo katika siku za hivi karibuni yamekuwa yakishuhudiwa humu nchini.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo polisi wamekuwa wakishutumiwa kwa kuwakandamiza waandamanaji wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z, ukandamizaji ambao umesababisha vifo vya makumi ya waandamanaji huku mamia ya wengine wakiuguza majeraha.
“Polisi wanapaswa kuitikia, kwa uwiano, na kuzingatia ipasavyo viwango vya haki za binadamu, na kuepukana na vitendo ambavyo vinaweza kusababisha madhara au vifo,” alishauri Jaji Koome wakati akiongoza uapisho wa makamishna wa Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi (NPSC) leo Jumanne.
“Pia ni wajibu wa polisi kutofautisha kati ya waandamanaji wa amani na wahalifu, wale wanaoingia kwenye maandamano ili kusababisha vurugu na uporaji na kuwashtaki watu kama hao kupitia mfumo wa sheria,” aliongeza Koome katika hafla iliyodhuhudiwa na Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, DCI Mohamed Amin.
Jaji Koome pia amewataka raia kufurahia haki yao ya kuandamana bila kubeba silaha na bila kushiriki vitendo vya kigaidi.
Aliyasema hayo wakati wa uapisho wa Peris Muthoni Kimani, Benjamin Juma Imai, na Prof. Collette Suda kama makamishna wa (NPSC), na Abdullahi Nur Sheikh Kassim mwanachama wa Baraza la Taifa la Mashujaa.
Awali, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen aliwalimbikizia maafisa wa polisi sifa sufufu kwa kudumisha utulivu wakati wa maandamano ya jana Jumanne.
Watu wasiopungua 10 walifariki wakati maandamano hayo huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.