Wabunge leo Alhamisi alasiri wanatarajiwa kupigia kura Mswada wa Fedha 2026 kwenye kikao kinachotarajiwa kujawa na cheche kali za maneno.
Ingawa wabunge wanaoegemea upande wa serikali wanaunga mkono mswada huo, wale wa upinzani wanaupinga vikali wakisema utasababisha Wakenya kutozwa ushuru wa kiwango cha juu ikiwa utapitishwa jinsi ulivyo.
“Mswada wa Fedha 2026/2027 uko mbele ya Bunge. Watu wa Kenya wanafuatilia na msimamo wao tayari unajulikana,” alisema kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka leo Alhamisi saa chache kabla ya mswada huo kupigiwa kura.
“Mswada huo haupaswi kupitishwa jinsi ulivyo sasa. Natoa wito kwa kila mbunge leo: wacha haki itawale. Pigia kura dhamira yako. Pigia kura mwananchi.”
Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua ambaye pia ni kinara wa chama cha DCP pia alielezea pingamizi zake kwa mswada huo.
“Kura ya leo katika Bunge la Taifa ya kuunga mkono au kupingfa Mswada wa Fedha 2026 ni kipindi muhimu kwa watu wa Jamhuri ya Kenya,” alisema Gachagua.
“Mwisho wa siku, Wakenya watafahamu ikiwa wabunge wao wanaunga mkono hatua zinazowakandamiza au zinazowajali.”
Gachagua amewataka wabunge wa DCP kukatalia mbali mswada huo.
Shirikisho la Watumiaji Bidhaa nchini, Cofek tayari limewasilisha kesi mahakamani kupinga baadhi ya vipengele tata kwenye mswada huo.
Kulingana na Cofek, mapendekezo ya kuiongezea nguvu Mamlaka ya Mapato nchini, KRA yanaweza kupalilia mbegu za utozaji ushuru bila kuzingatia mizani ya haki, ikiwa ni pamoja na wanaotozwa ushuru kutosikilizwa.
Kadhalika, linasema hatua ya kuondoa msamaha wa Ushuru Ziada wa Thamani, VAT kwa baadhi ya bidhaa itapisha kupanda kwa bei za vyakula na vifaa tiba miongoni mwa mambo mengine.
Upande wa serikali umepuuzilia mbali madai hayo ukiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.