Harambee Starlets wateketeza nge wa Gambia, wanusia fainali za WAFCON

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka kwa wanawake almaarufu Harambee Starlets imejiweka katika nafasi bora ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON) mwaka ujao, baada ya kuwashinda Gambia mabao 3-1 katika mkumbo wa kwanza raundi ya pili uliopigwa ugani Nyayo Ijumaa alasiri.

Wageni, The Scorpions, walichukua uongozi wa dakika ya pili kupitia kwa Fatoumatah Kentah, kabla ya Mwanahalima Adam kuwarejesha wenyeji mchezoni kwa goli la kusawazisha dakika ya 12 kupitia mkwaju wa penati kabla ya Fasila Adhiambo kuiweka Kenya uongozi dakika saba baadaye.

Shalyne Opisa alihitimisha kibarua kwa Kenya kwa bao la dakika ya pili ya muda wa mazidadi kipindi cha kwanza.

Mechi ya marudio itasakatwa Jumanne ijayo nchini Senegal huku mshindi akifuzu kwa fainali za WAFCON zitakazoandaliwa mwezi Machi mwakani nchini Morocco.

Kenya inalenga kufuzu kwa WAFCON kwa mara ya pili tangu iliposhiriki mwaka 2016 nchini Cameroon.

Timu hiyo itatuzwa shilingi milioni 5 kutoka kwa Rais William Ruto kufuatia ushindi wa Ijumaa.

Website |  + posts
Share This Article