Hali ya tahadhari imetangazwa katika jiji la New York nchini Marekani kufuatia dhoruba iliyosababisha mafuriko ya muda.
Vituo vingi vya gari moshi jijini humo, barabara ndogo na barabara kuu zilijaa maji huku kituo kimoja kikifungwa katika uwanja wa ndege wa LaGuardia kabla ya kufunguliwa tena Ijumaa.
Gavana Kathy Hochul alitaja dhoruba hiyo kuwa ya kutishia maisha huku akitangaza hali ya dharura katika jiji la New York, eneo la Long Island pamoja na Hudson Valley kwa sababu ya kiwango cha juu cha mvua.
Alisihi wakazi wa maeneo hayo kuchukua hatua za kujuhakikishia usalama lakini akawashauri wasisafiri kwenye barabara zilizofurika.
Alisema hakuna kifo kiliripotiwa kutokana na hali hiyo.
Hali ya tahadhari ilitangazwa pia katika mji wa Hoboken jimboni New Jersey ng’ambo ya mto Hudson.
Mvua hiyo kubwa ilipoa lakini viongozi wanazidi kuhimiza wakazi kuwa macho.