Gor wabanwa huku Tusker wakishinda mechi za kufungua ligi kuu

Dismas Otuke
1 Min Read

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Kenya,Gor Mahia wametoka nyuma na kulazimisha sare ya bao 1 dhidi ya Sofapaka, katika mchuano wa kufungua msimu wa mwaka 2023/2024 uliosakatwa katika uga wa Kasarani siku ya Jumamosi.

Darius Msagha aliwaweka Sofapaka kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya Benson Omalla kusawazishia The Green Army kupitia penati ya dakika ya 82.

Tusker FC walikosa adabu za mgeni walipobwaga wenyeji Bandari FC bao 1 kwa sifuri ugani Mbaraki Sports kupitia kwa goli lake James Kibande katika dakika ya 42.

Kwenye matokeo mengine Nzoia Sugar wakiwa nyumbani kiwarani sudi wameilaza Ulinzi Stars mabao 2-1 huku police FC na Kariobangi Sharks wakiumiza nyasi bila lengo kwa kutoka sare kappa.

Michuano minne zaidi ya kuhitimisha raundi ya kwanza kusakatwa Jumapili Posta Rangers wakiwaalika Bidco United katika uga wa Kasarani,wakati AFC Leopards wakipimana nguvu na Talanta FC katika uwanja wa Nyayo.

Muhoroni Youth watawatembelea Nairobi City Stars katika uwanja wa Kasarani Annex kisha Shabana FC wafungue msimu nyumbani dhidi ya Murang’a Seal katika uchanjaa wa Raila Odinga.

Share This Article