Naibu Rais Rigathi Gachagua ameonya dhidi ya kutumiwa kwa mfumo wa sheria kudhibiti siasa nchini.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI imeashiria mipango ya kuwafungulia wandani wake wa kisiasa mashtaka ya kuchochea au kufadhili maandamano ya vijana wa Gen Z yaliyoshuhudiwa humu nchini miezi michache ilyopita.
Miongoni mwa wanasiasa wanaolengwa ni mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiri Mwangi, James Mwangi Gakuya (Embakasi North), George Theuri (Embakasi West) na aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.
“Njama hii potovu inakusudia kuwahusisha na ghasia zenye vurugu zilizoshuhudiwa nchini mwishoni mwa mwezi Juni katika jaribio la kunichafulia jina kwa matumaini ya kutafuta sababu za kunitimua madarakani,” alisema Naibu Rais kupitia mtandao wake wa X.
“Wakenya ni watu werevu. Wanafahamu vigezo vilivyosababisha kuzuka kwa maandamano. Wakenya pia wanafahamu matatizo halisi yanayoikumba nchi hii. Ziache taasisi zetu ziendeshe mambo yao kitaaluma, zifuate utawala wa sheria na ziachane na siasa.”
Kulingana na Gachagua, matumizi ya mfumo wa sheria kudhiti siasa za nchi ni mkakati wa kisiasa uliotumiwa zamani na ambao umepitwa na wakati.
Tofauti za kali za kisiasa zimeibuka kati ya Rais William Ruto na Gachagua kiasi kwamba wabunge wanaoegemea mrengo wa Rais wanapanga kuwasilisha hoja ya kumtimua madarakani.