Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inataka wabunge wanaoshukiwa kupanga na kufadhili maandamano ya vijana wa Gen Z yaliyoshudiwa nchini mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu kufunguliwa mashtaka.
Wabunge hao ni pamoja na mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiri Mwangi, James Mwangi Gakuya (Embakasi North), George Theuri (Embakasi West) na aliyekuwa mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu.
Mwingine aliyetajwa kwenye barua ya DCI iliyoandikwa na Abdallah Komesha kwa niaba ya idara hiyo ikitafuta ushauri wa Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuhusiana na mapendekezo ya jumla ya washukiwa hao saba kufunguliwa mashtaka ni Pius Munene.
Wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga, kuchochea au kufadhili maandamano hayo huku mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiri Mwangi akikabiliwa na mashtaka mengi ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha.
“Juhudi zinafanywa kupata taarifa za kifedha kutoka kwa FRC, kampuni ya Safaricom na benki ambako miamala ya kifedha ilifanywa,” anasema Komesha katika barua yake kwa ODPP.
Wabunge wote wanaotuhumiwa kwa kufadhili maandamano ya vijana wa Gen Z ni wandani wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Tayari Gachagua amelaani vikali mapendekezo ya kushtakiwa kwao akiitaja kuwa njama ya kumhusisha na maandamano hayo wakati mihemko ya kutimuliwa kwake madarakani imepamba moto.
“Njama hii potovu inakusudia kuwahusisha na ghasia zenye vurugu zilizoshuhudiwa nchini mwishoni mwa mwezi Juni katika jaribio la kunichafulia jina kwa matumaini ya kutafuta sababu za kunitimua madarakani,” alisema Naibu Rais kupitia mtandao wake wa X.
“Wakenya ni watu werevu. Wanafahamu vigezo vilivyosababisha kuzuka kwa maandamano. Wakenya pia wanafahamu matatizo halisi yanayoikumba nchi hii. Ziache taasisi zetu ziendeshe mambo yao kitaaluma, zifuate utawala wa sheria na ziachane na siasa.”