Naibu Rais aliyeng’atuliwa afisini na bunge la Seneti Rigathi Gachagua, amejitokeza kimasomaso kwa mara ya kwanza na kusema kuwa amepata afueni baada ya kulazwa katika hospitali ya Karen.
Akihutubia Wanahabari punde baada ya hotuba ya Rais ya Sikukuu ya Mashujaa katika uwanja wa Kwale, Gachagua ameelezea matumaini ya kupata haki mahakamani kwenye kesi aliyopinga kutimuliwa, huku akisisitiza kuwa angali Naibu Rais wa Kenya.
Gachagua alikosa kufika mbele ya bunge la Seneti Alhamisi iliyopita kutoa utetezi wake dhidi ya kubanduliwa afisini baada ya kulazwa kwa maumivu.
Bunge la Seneti lilitupilia mbali ombi la wakili wake kutaka uamuzi uahirishwe hadi Jumanne wiki hii ili kumruhusu Gachagua kujitetea.
Tayari bunge la kitaifa limemwidhinisha Waziri wa Usalama wa Kitaifa Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais kumrithi Gachagua.
Hata hivyo, mahakama kuu imesimamisha uapisho wake hadi pale kesi ya mtangulizi wake itakaposikizwa na kuamuliwa.