Gachagua afungua kongamano la kimataifa la sayansi la wanafamasia

Marion Bosire
1 Min Read

Naibu rais Rigathi Gachagua hivi leo ameongoza ufunguzi wa kongamano la kimataifa la sayansi la wanafamasia huko Mombasa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, naibu rais alisema kwamba serikali imejitolea kuhakikisha kuafikiwa kwa haraka kwa mpango wa afya bora kwa wote ili kuwa na nchi yenye afya.

Kiongozi huyo alisema kwamba jukumu la kila mtaalamu wa sekta ya afya wakiwemo wanafamasia katika kuafikia mpango huo wa afya bora kwa wote ni muhimu sana ili kuafikia ufanisi.

Kwa niaba ya rais William Ruto na serikali kwa jumla, Gachagua alipongeza chama cha wanafamasia kinapoadhimisha miaka 60 tangu kilipobuniwa.

“Mnaposherehekea ufanisi huu, hakikisho letu kwenu ni kwamba tuko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha viwango vya kitaalamu vinazingatiwa katika sekta yenu, tunapotafuta kuwa na huduma bora za afya kwa wote na kwa bei nafuu.” alisema Gachagua.

Naibu rais alikuwa ameandamana na waziri wa afya Susan Nakhumicha, rais wa chama cha kimataifa cha wanafamasia Profesa Lisa Pont, rais wa chama cha wanafamasia wa Kenya Daktari Somoni Machogu na wengine.

Kongamano la mwaka huu la kimataifa la sayansi la wanafamasia linaandaliwa katika hoteli ya Sarova Whitesands Mombasa. Lilianza juni 10 na litafikia kikomo juni 14, 2024.

Website |  + posts
Share This Article