Wananchi wahimizwa kuchukua tahadhari wakati huu wa msimu wa mvua

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga.

Huku maeneo mbali mbali ya taifa hili yakiendelea kushuhudia msimu wa mvua za vuli, Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko, maporomoko ya ardhi na barabara telezi.

Chidzuga alisema serikali itakabiliana na hali za dharura ambazo huenda zikasababishwa na mvua inayoendelea kunyesha hapa nchini.

Kupitia taarifa siku ya Jumamosi kwenye ukurasa wa X, saa chache baada ya watu kadhaa kuthibitishwa kufariki kutokana na maporomoko ya ardhi kaunti ya Elgeyo Marakwet, Chidzuga alisema taifa hili litaendelea kushuhudia mvua ya kiwango cha juu, na kusababisha uwezekano wa mafuriko.

Aidha aliomboleza na familia zilizowapoteza wapendwa wao kwenye mkasa huo wa maporomoko ya ardhi, akiahidi usaidizi wa serikali katika shughuli inayoendelea ya uokoaji.

“Kama serikali tumesikitishwa na kupotea kwa maisha na tunaomboleza na familia zilizowapoteza wapendwa wao,” alisema Chidzuga.

Alidokeza kuwa serikali tayari imepeleka helikopta kusaidia kuwasafirisha maafisa wa kukabiliana na dharura wanaosaidia katika shughuli za uokoaji.

Watu kadhaa wamethibitishwa kufariki huku wengine wengi wakiripotiwa kutoweka kufuatia maporomoko makubwa ya ardhi yaliyotokea Murkutwa, Chesongoch, kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Website |  + posts
Share This Article