Jacky Ndala ambaye ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya DRC amehamishiwa gereza la kijeshi la Ndolo nchini DRC, hatua inayozua mjadala mpana kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari, Ndala anakabiliwa na tuhuma za kuwa na uhusiano na kundi la Waasi la AFC/M23, ambalo limekuwa likihusishwa na machafuko katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Chanzo cha taarifa hiyo kilieleza kuwa, “Jacky Ndala amehamishiwa katika Gereza la kijeshi la Ndolo na anashitakiwa kwa kudumisha uhusiano na uasi wa AFC/M23.”
Hata hivyo, hadi sasa hakuna kauli rasmi iliyotolewa na mamlaka ya Serikali kuthibitisha kwa kina tuhuma hizo, huku wafuasi wa Mwanasiasa huyo wakieleza wasiwasi wao juu ya usalama wake na mchakato wa kisheria unaomkabili.
Kesi hiyo inakuja wakati hali ya usalama mashariki mwa DRC ikiendelea kuwa tete, huku serikali ikikabiliana na makundi mbalimbali ya Waasi, likiwemo lile la M23 ambalo limekuwa likiripotiwa kuimarisha shughuli zake katika miezi ya hivi karibuni.
Ndala ambaye amekuwa akijikuta pabaya kisheria ambapo amekamatwa na kuhukumiwa vifungo gerezani mara kadhaa alikamatwa Machi 7, 2026, kwa tuhuma za kushirikiana na waasi wa AFC/M23.