Filamu ya Bobi Wine yateuliwa kuwania tuzo za Oscar

Marion Bosire
2 Min Read

Filamu ya matukio halisi “Bobi Wine: The People’s President” imeteuliwa kuwania tuzo za Oscar katika kitengo cha filamu bora ya matukio halisi au ” Best Documentary Feature”.

Taarifa kuhusu uteuzi wa kazi hiyo kuwania tuzo zinazoenziwa zaidi ulimwenguni zilimpata Wine akiwa amejifichia maafisa wa polisi.

Maafisa hao wa polisi walikuwa wamezingira makazi yake baada ya kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha National Unity Platform – NUP kuitisha maandamano kulalamikia mfumo duni wa barabara nchini Uganda.

Anasema kwamba alipiga nduru alipojuzwa kwamba kazi hiyo imeteuliwa akitania kwamba maafisa wa polisi wangekuwa karibu wangemkamata.

Filamu hiyo inaangazia kipindi cha miaka mitano cha maisha ya Wine kuanzia alipochaguliwa kuwa mbunge wa eneo la Kyadondo Mashariki hadi alipowania uchaguzi wa urais.

Iliandaliwa na kampuni ya Southern Films Ventureland na kuhusisha waandalizi wa filamu John Battsek na Christopher Sharp.

Sharp alihudumu pia kama mwelekezi wa filamu hiyo akisaidiwa na Moses Bwayo huku kazi hiyo ikisambazwa na “National Geographic Documentary Films”.

Kazi hiyo ya dakika 113 ilizinduliwa Septemba 1, 2022 huko Venice na Julai 28, 2023 nchini Marekani na inaaminika kupata mapato ya dola elfu 44,486 kwenye Box office.

Hafla ya kutuza washindi wa vitengo mbali mbali vya tuzo za Oscar awamu ya 96 inatarajiwa kuandaliwa kwenye ukumbi wa maonyesho wa Dolby huko Hollywood, Los Angeles, California, nchini Marekani Machi 10, 2024.

Website |  + posts
Share This Article