Shirika la FAWE Kenya limeelezea mashaka juu ya idadi kubwa ya wasichana wasioenda shuleni mjini Garissa na kutoa wito wa kufanywa kwa juhudi za pamoja kukabiliana na hali hiyo.
Utafiti uliofanywa mwaka 2022 ulibaini kuwepo kwa idadi ndogo ya wasichana wanaohudhuria masomo katika kaunti ya Garissa ambayo ni asilimia 11.
Harrison Ochola ni mratibu wa FAWE Kenya katika kaunti ya Garissa. Amesema takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 20 pekee ya wasichana wanaonufaika na masomo katika kaunti hiyo huku wanafunzi waliosalia wakiwa wavulana.
Aliyasema hayo pembezoni mwa mkutano wa mapitio ya Mradi wa Imarisha Msichana ambao unatekelezwa na FAWE Kenya kwa ushirikiano na shirika la MasterCard Foundation.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Walimu Wakuu, walimu pamoja na wanafunzi.
Ochola alitoa wito kwa serikali na mashirika mengine yasiyokuwa ya serikali kuunga mkono kikamilifu elimu ya watoto wasichana ambao alisema idadi yao bado ni ndogo ikilinganishwa na wavulana.
“Ukiangalia tafiti zilizofanywa, zote zinaelezea taswira mbaya ya elimu ya wasichana wetu. Idadi yao shuleni ni ndogo. Hii inapaswa kuwatia hofu washikadau wote,” alisema Ochola.
Baadhi ya vikwazo vya elimu ya wasichana nchini ni tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji.