Faith Odhiambo ajiuzulu kutoka jopo la fidia

Martin Mwanje
2 Min Read
Faith Odhiambo - Rais wa LSK

Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK, Faith Odhiambo ametangaza kujiuzulu kutoka kwenye jopo la fidia kwa waathiriwa wa maandamano tangu mwaka 2017. 

Odhiambo ametangaza kujiuzulu kwake kwenye taarifa leo Jumatatu,  takriban mwezi mmoja baada ya hatua yake ya kuridhia kuhudumu kwenye jopo hilo kukabiliwa na shutuma kali kutoka kwa baadhi ya Wakenya.

“Jinsi tu ambavyo azimio la Chama cha Wanasheria nchini Kenya limekuwa thabiti katika kudumisha utawala wa sheria katika kipindi chote cha historia ya Kenya, hasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kiapo cha ofisi yangu kinanihitaji kufanya kila liwezekanalo kulinda uthabiti kama huo dhidi ya kuingiliwa na adui au mkashifishaji yeyote,” alisema Odhiambo.

“Kwa misingi hiyo, hii leo nimepatiana kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma barua yangu rasmi ya kujiuzulu kutoka kwenye wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa Jopo la Wataalam Juu ya Ulipaji Fidia kwa Waathiriwa wa Maandamano.”

Amesema ataendelea kupigania haki za waathiriwa hao kupitia LSK.

Jopo hilo linaloongozwa na mshauri wa Rais William Ruto kuhusiana na masuala ya kikatiba Prof. Makau Mutua lilipaswa kutekeleza wajibu wake ndani ya siku 120.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Kerugoya ilipiga breki utenda kazi wa jopo hilo baada ya wakili Levi Munyeri kuelekea mahakamani kupinga uhalali wake.

Ni kesi ambayo imelemaza utenda kazi wa jopo hilo hadi sasa, hata ingawa jopo hilo lilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Ilivyo kwa sasa, hatima ya jopo hilo haijulikani.

Website |  + posts
Share This Article