Ezekiel Mutua amkosoa Ssaru kwa wimbo usio na maadili

Marion Bosire
2 Min Read

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki za Muziki Nchini, MCSK Daktari Ezekiel Mutua anaendelea kumkosoa mwanamuziki wa mtindo wa rap Sylvia Ssaru kwa wimbo wake “Kasikie vibaya huko kwenu” ambao anahisi umekiuka maadili ya jamii. Awali, Mutua alikuwa ameukosoa wimbo huo kwa maneno machache tu kupitia akaunti yake ya Facebook na akajibiwa na Ssaru.

Mara ya pili, Mutua ambaye anafahamika kwa kulinda maadili ya jamii katika sekta ya burudani aliandika makala marefu kwenye Facebook akimzomea Ssaru kwa kukosa kutilia maanani ukosoaji kutoka kwa watu wanaomzidi umri na badala yake akachagua kufurahisha wafuasi wake mitandaoni.

Kulingana naye, wafuasi wa mitandaoni watasifu wimbo huo kwa muda tu hadi watakapopata mwingine wa kusikiliza.

Dkt. Mutua alimwonya Ssaru kwamba kampuni kubwa huenda zikamsusia kutokana na kutozingatia maadili ya jamii katika nyimbo zake na hivyo atakosa kazi ambazo zingempa mapato mengi.

Alitetea ukosoaji wake wa mwanamuziki huyo akisema unatokana na mapenzi na ukweli na anataka kuhakikisha kwamba Ssaru na wanamuziki wengine wanaandaa kazi ambazo zitasikilizwa na wote.

Dkt. Mutua anahisi kwamba wimbo “Kasikie vibaya huko kwenu” ambao amemshirikisha Father Moh, unaendeleza ukosefu wa maadili katika jamii.

Ssaru anasisitiza kwamba yeye hutayarisha kazi mbalimbali za sanaa kulingana na mahitaji ya makundi mbalimbali ya wasikilizaji.

Alimsihi Dkt. Mutua ajifahamishe na nyimbo zake kabla ya kumhukumu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *