Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi amesema kwamba alizuiwa kusafiri nje ya nchi.
Alichapisha taarifa hizo kwenye akaunti yake ya mtandao wa X akisema alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kabla ya kuabiri ndege kuelekea Dar es Salaam nchini Tanzania.
Safari hiyo ilikuwa ya kuazisha safari za ndege za kampuni ya Skyward kuelekea Tanzania. Anahudumia kampuni hiyo kama balozi.
“Nilipowapa maafisa wa uhamiaji paspoti yangu, walinijuza kwamba kuna agizo la kunizuia nisiondoke nchini na kwamba ni lazima nizuiliwe.” aliandika Omondi kwenye X.
Ujumbe huo ulisababisha wafuasi wake kwenye mtandao huo waanzishe wito wa kutaka aachiliwe huru, huku wachache wakichukuliwa ujumbe wake kuwa wa kutafuta kuangaziwa mitandaoni tu.
Omondi ni mmoja kati ya watu maarufu nchini ambao wamekuwa wakipendekeza mabadiliko ya uongozi kutokana na kile anachosema kuwa ni uongozi mbaya.