Msanii wa muziki nchini Kenya Bien Barasa na mwenzake wa Tanzania Diamond Platnumz wametoa kazi yao ya pamoja kwa jina ‘Katam’.
Wimbo huo mtamu wa mapenzi umeunganisha wasanii wawili wakubwa wa Afrika Mashariki kusherehekea urembo, mapenzi na umoja katika bara hili .
Unasimulia kuhusu mwanamke mmoja wa kipekee ambaye urembo wake huduwaza wengi kwani ana msisimko mzuri, umbo zuri na kila kitu kizuri ndiposa wakamrejelea kama katamu.
Wimbo huo ambao ulitayarishwa na S2Kizzy mtayarishaji maarufu wa muziki nchini Tanzania unapatikana kwenye majukwaa yote ya mtandaoni.
Katika maneno yao na sauti zao za kupendeza wasanii hao wawili wanaleta picha ya mwanamke anayeonyesha uzuri wa eneo la Afrika Mashariki ambapo wanazungumzia mng’ao wa ngozi wa Rwanda, nywele za ki-Somali, Macho ya Ethiopia, utamu wa Tanzania na werevu wa Kenya.
Ushirikiano huu unajiri yapata miaka minne tangu Bien aliposema kwamba amerekodi wimbo pamoja na Diamond.
Katika mahojiano na jukwaa moja la habari la Kenya mwezi Juni mwaka 2021, Bien ambaye alikuwa amerejea kutoka Tanzania ambapo alikutana na Diamond wakati huo alisema walirekodi wimbo.
Katika ziara hiyo, Bien alikuwa ameandamana na Eugene Mbugua ambaye anafahamika sana kwa utayarishaji wa vipindi vya matukio halisi vinavyohusisha watu maarufu.