Duale: Tutatekeleza sheria zote za kuhifadhi mazingira

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Mazingira Aden Duale.

Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Misitu Aden Duale amekariri kujitolea kwa serikali kutekeleza kikamilifu sheria zote za mazingira, ikiwa ni pamoja na zile zinazotoa mwongozo kuhusu utupaji taka na ulinzi wa mazingira.

Duale alitoa hakikisho hilo alipofika mbele ya kamati ya bunge kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mambo ya Nje, kujibu maswali ya kimazingira kutokana na mazoezi ya kitengo cha wanajeshi wa Uingereza hapa nchini (BATUK) katika kaunti za Samburu na Laikipia.

Katika mkutano huo ulioongozwa na mbunge wa Belgut Nelson Koech, waziri huyo alisema wizara yake imetoa agizo kwa BATUK kutunza mazingira, ambapo wachunguzi wa Halmashauri ya Usimamizi wa Mazingira nchini, NEMA watakagua vituo vya mazoezi vya wanajeshi hao.

Kulingana na Duale, agizo hilo linahitaji BATUK kutoka rekodi za ilani zote za kimazingira katika muda wa miaka tano iliyopita, ikiwa ni pamoja na vyanzo vyao na hatua za zilizochukuliwa kurekebisha hali, katika muda wa siku saba zijazo.

Duale, aliyekuwa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya NEMA Mamo Mamo na mkuu wa kitengo cha sheria katika wizara hiyo Annie Syombua, alirejelea kusema kuwa taasisi zote za hapa nchini na zile za kimataifa zinazoendesha shughuli ambazo ni hatari kwa mazingira, ni sharti zizingatie sheria ya kudhibiti mazingira ya mwaka 1999.

Alielezea kujitolea kwa wizara yake kuhakikisha jutandu wa msitu wa asilimia 30 kufikia mwaka 2032, kupitia mpango wa upanzi wa miti bilioni 15 unaotekelezwa na serikali ya Kenya Kwanza.

Share This Article