Diddy akanusha mashtaka yaliyorekebishwa dhidi yake

Mawakili wa Diddy wanasema madai hayo yanahusu mahusiano ambayo wahusika walikubaliana hasa na wapenzi wake wa kike.

Marion Bosire
2 Min Read
P Diddy

Mwanamuziki Sean “Diddy” Combs alikanusha mashtaka dhidi yake ambayo yalifanyiwa marekebisho yanayojumuisha madai ya kufanya watu watumwa.

Kulingana na mashtaka hayo, Diddy anadaiwa kulazimisha wafanyakazi wake kuhudumu kwa muda mrefu huku akitishia kuwadhuru moja kwa moja au kudhuru sifa zao.

Anaripotiwa pia kulazimisha mfanyakazi mmoja kushiriki vitendo vya kingono naye.

Mawakili wa Diddy walikanusha madai hayo wakisema yanahusu mahusiano ambayo wahusika walikubaliana hasa na wapenzi wake wa kike.

Walikanusha pia madai kwenye kesi ambazo zimewasilishwa mahakamani dhidi yake katika miezi ya hivi karibuni.

Wakili Marc Agnifilo alisema kwamba mwanamuziki huyo anasubiri kwa hamu kubwa siku ambayo atafika mahakamani ambapo itabainika kwamba hakuwahi kulazimisha yeyote kushiriki ngono naye.

Combs anakabiliwa na kesi kadhaa ambapo walalamishi wanadai kubakwa na kudhulumiwa naye, kesi ambazo mawakili wake wamepuuza wakisema walalamishi wanajitafutia makuu.

Alitiwa mbaroni Jumatatu Septemba 16, 2024 kwa makosa ya dhuluma za kingono dhidi ya watu mbali mbali ambazo alitekeleza katila muda wa miaka mingi.

Tangu wakati huo, mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya Bad Boy Records, amesalia kizuizini huku akinyimwa dhamana mara kadhaa.

Sababu kuu ya mahakama kumyima dhamana ni uwezekano wake kuingilia au kudhuru mashahidi wa kesi dhidi yake. Kesi hiyo imepangiwa kuanza kusikilizwa rasmi mwezi Mei mwaka huu wa 2025.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *