Daktari Denis Masoba Nyambane wa umri wa miaka 36 aliyekamatwa kwa madai ya kumuua mkewe Mary Mwende Mutie wa miaka 30, atasalia kizuizini kwa siku 7 zaidi wapelelezi wa kaunti ya Kiambu wakikamilisha uchunguzi.
Denis ambaye ni mtaalamu wa upasuaji katika Hospitali ya Kiambu Level 5, anadaiwa kumchoma mke wake Mary kisu cha jikoni katika nyumba yao ya kupanga iliyoko Busacarde Plaza, Kiambu.
Polisi wanasema Mwende alifariki papo hapo, akiacha mtoto wao wa kiume wa miaka mitatu, ambaye sasa amepatwa na mshtuko wa kihisia kutokana na tukio hilo.
Wakati wa ukaguzi katika eneo la tukio, madoa ya damu yalipatikana kwenye ngazi, ambapo inaaminika marehemu alianguka alipokuwa akijaribu kutoka nje ya nyumba baada ya kupata majeraha ya kuchomwa kisu.
Msimamizi wa jengo hilo, Isaac Omare, alisema aliarifiwa na jirani aliyepiga simu kuomba msaada baada ya Mwende kuchomwa kisu. Hata hivyo alipofika, alipata tayari alikuwa amefariki, hivyo wakaarifu Kituo cha Polisi cha Kiambu.
Omare alisema familia hiyo ilikuwa imeishi katika nyumba hiyo kwa takribani wiki mbili pekee baada ya kuhama kutoka makazi ya karibu, na haikuwa imezoeana sana na wapangaji wengine.
Jirani yao aitwaye Costan Wangui alisema wakazi walikimbia kutoa msaada lakini wakamkuta Mwende akiwa amelala kwenye dimbwi la damu huku mtoto wake mdogo akiwa pembeni.
Mshukiwa atafanyiwa uchunguzi wa afya ya akili katika Hospitali ya Kiambu, huku uchunguzi wa maiti ukifanywa katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta ili kubaini chanzo cha kifo.