Mashirika ya habari yamshtaki Trump

Yanalalamikia hatua ya Trump ya kuuza ufikiaji wa mapema wa machapisho yake, kwenye mtandao wake wa Truth Social.

Marion Bosire
3 Min Read

Jarida la mitandaoni la ‘The Intercept’ na wakfu usio wa faida kuhusu uhuru wa vyombo vya habari zimefungua kesi dhidi ya Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mashirika hayo mawili yanataka kuzuia huduma ya Trump ya mitandao ya kijamii kuuza ufikiaji wa mapema wa machapisho yake.

Nyaraka za mahakama zilizowasilishwa Jumatano zinasema kuwa huduma hiyo inayotumia mfumo wa usajili itazuia upatikanaji wa taarifa zinazohusu masuala muhimu kwa umma.

Katika malalamiko yao, mashirika hayo yalitaja mpango huo kuwa uliooza kwa kiwango kikubwa.

Kesi hiyo inarejelea haki ya uhuru wa vyombo vya habari chini ya Katiba ya Marekani na inasema mpango huo utakiuka Marekebisho ya Kwanza ya Katiba, ambayo yanaweka dhamana ya kimsingi ya “upatikanaji sawa wa matangazo ya umma ya Rais.”

Pia inadai kuwa huduma hiyo ya usajili itakiuka ulinzi unaotolewa na Marekebisho ya Tano ya Katiba, ambayo, kwa mujibu wa kesi hiyo, yanaizuia serikali kutoza fedha kiholela ili watu wapate taarifa za serikali.

Malalamiko hayo yanamtaja Trump kwa nafasi yake rasmi, pamoja na msaidizi wa Ikulu Natalie Harp na Naibu Mkuu wa Watumishi Daniel Scavino.

Kesi hiyo inalenga Truth API, huduma iliyotangazwa mwezi Julai na kuanza kutumika Agosti 1.

Huduma hiyo ya usajili, ambayo ni bidhaa ya Trump Media and Technology Group, inawatoza watumizi kati ya dola 60,000 na 100,000 kwa mwezi ili kupata kwa wakati halisi machapisho kutoka kwa Trump na akaunti nyingine mashuhuri kwenye Truth Social, jukwaa la mitandao ya kijamii la kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa malalamiko hayo, zaidi ya wateja 10 walikuwa tayari wamejisajili.

Wakosoaji wameeleza kuwa Trump hutumia akaunti yake ya Truth Social kutangaza mabadiliko ya sera ambayo yanaweza kuathiri uchumi. Kwa mfano, kauli za Trump kuhusu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran zimesababisha mabadiliko katika masoko ya mafuta duniani.

“Trump anajaribu kujitajirisha kwa kubinafsisha taarifa za serikali ambazo hana haki ya kuziuza,” alisema Ben Muessig, mhariri mkuu wa The Intercept akiongeza “Hatutakubali jambo hilo liendelee.”

Trump Media ilisema katika taarifa kwamba mawasiliano ya rais tayari hupitia “majukwaa na vyombo vingi vya habari, ambavyo vingi vinatoa huduma kwa usajili na malipo.”

Ikulu ya Marekani haijatoa maoni kuhusu mzozo huo. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa katika mahakama ya shirikisho ya Southern District of New York.

Share This Article