COSAFA 2024: Kenya yashinda Zimbabwe kukaribia nusu fainali

Marion Bosire
2 Min Read

Kenya imepata ushindi wa 2 – 0 kwenye mashindano ya COSAFA 2024 kule Afrika Kusini dhidi ya Zimbabwe uwanjani Wolfson, Port Elizabeth Jumanne.

Mechi hiyo ilikuwa ya kukamilisha awamu ya makundi katika Kundi B. Mabao hayo mawili yalifungwa katika kipindi cha pili.

Austin Odhiambo na Benson Omalla wote wakichezea Gor Mahia walifunga mabao hayo dakika za 54 na 73 mtawalia. Odhiambo alipokea tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Hiyo ilikuwa mechi ya pili kwa Kenya kusajili ushindi. Kwenye mechi ya kwanza, walishinda Zambia 2 – 0. Walipoteza mechi ya pili ya makundi walipochapwa 2 – 0 na Comoros.

Kutokana na matokeo hayo, Kenya ina alama sita katika Kundi B sawa na Comoros ambayo ilisajili ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Zambia Jumanne pia. Zimbabwe inakalia nambari ya tatu na alama sita ikiwa inadunishwa na idadi ya mabao. Zambia iko mkiani bila alama yoyote.

Matumaini ya Kenya kufuzu kwa nusu fainali inategemea matokeo ya timu za Angola na Namibia. Timu hizo zina alama nne katika Kundi C. Lazima timu moja ipoteze mechi ya mwisho siku ya Jumatano ili Kenya ifike nusu fainali ikiwa timu bora iliyomaliza ya pili.

Timu moja ya kwanza itafuzu nusu fainali moja kwa moja. Kwa kuwa ni makundi matatu, timu ya pili itachaguliwa kutoka kwenye orodha ya timu nambari ya pili bora.

Angola itacheza na Lesotho huku Namibia ikipambana na Seychelles.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *