Chiwetalu Agu amsifia Yemi Alade

Yemi Alade alihudhuria hafla ya tuzo za Grammy akiwa amevaa vazi asilia la Nigeria.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji mkongwe wa Nigeria Mzee Chiwetalu Agu amemsifia mwanamuziki wa Nigeria Yemi Alade kwa kuwakilisha asili yake ipasavyo.

Mzee huyo alichapisha video kwenye Instagram na kuiambatanisha na picha ya Yemi Alade akiwa kwenye hafla ya kutoa tuzo za Grammy nchini Marekani na kumrejelea kama Malkia.

“Yemi Alade wewe ni Malkia, Malkia unavyojifikiria.” alisema Agu kwenye video hiyo na kuendelea kuelezea jinsi binti huyo aliwakilisha mtindo wa Afrobeat.

Alisema hata kama Yemi hakushinda tuzo ya Grammy, alijishindia nafasi nzuri katika moyo wake kutokana na hatua yake ya kuwakilisha utamaduni wa Afrika kutokana na vazi lake.

Hatua ya Yemi anasema iliweka utamaduni wa Afrika kwenye ramani ya ulimwengu.

“Vazi lake lilikuwa linasema sikuja hapa kuwafurahisha, ninafahamu asili yangu.” alisema Agu kwenye video hiyo huku akihimiza Yemi aendelee kumotisha wanawake.

Yemi Alade alikuwa ameteuliwa kuwania tuzo ya Grammy katika kitengo cha tumbuizo bora la muziki wa Afrika katika awamu ya 67 ya tuzo hizo.

Alifika huko akiwa amevaa vazi asilia la Nigeria la rangi nyekundu ambalo aliambatanisha na vito vya kiafrika.

Mwanamuziki huyo alikuwa akishindana na wanamuziki wa Nigeria kwenye kitengo hicho wakiwemo Asake, Wizkid, Chris Brown, Burna Boy na Tems ambaye aliibuka mshindi.

Website |  + posts
Share This Article