Serikali imetoa tahadhari ya uwezekano wa kufurika kwa bwawa la Masinga katika siku zijazo, huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha kote nchini.
Waziri wa kawi Davis Chirchir, amesema bwawa hilo huenda likavunja kingo zake katika kipindi cha wiki moja, huku akisikitikia hali ilivyo katika Kaunti ya Tana River ambayo imeathirika pakubwa kutoka na mafuriko.
“Kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa, mabwawa yetu ya uzalishaji umeme hasaa Masinga yanapokea viwango vikubwa vya maji. Bwawa la Masinga kwa sasa lina mita 1,047.51 za maji juu ya wastani wa bahari, dhidi ya kiwango cha maji kinachostahili cha mita 1,056. Tumesalia na mita tisa pekee za maji ili kifikie kiwango cha maji kinachoweza kuhifadhiwa na bwawa hilo,” alisema Waziri Chirchir.
Waziri huyo ambaye siku ya Ijumaa alifanya ziara ya kukagua mabwawa ya KenGen Seven Forks kutathmini viwango vya maji, aliwahimiza Wakenya wanaoishi katika maeneo ya chini ya Mto Tana, kuhama mara moja, huku mbunge wa Garissa Dekow Baro akisema kwamba kuvunjika kwa kingo za bwawa hilo kutaathiri vibaya miji iliyofurika.
“Hii inamaanisha kuwa bwawa hilo litafurika mwishoni mwa wiki au mapema wiki ijayo iwapo mvua itaendelea kunyesha. Tunawasihi wale wanaosihi karibu na bwawa hilo kuhamia maeneo salama kuepusha maafa na kupunguza uharibifu wa mali,” aliongeza waziri huyo.
Bwawa la Masinga husambaza maji yake kwa mabwawa mengine manne ambayo pia yako karibu kujaa maji.