Billnass asimulia alivyoachana na uganga

Alikamatwa na polisi muda mfupi tu baada ya kutembelea mganga aliyemhakikishia kwamba hangekamatwa.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muziki na mfanyabiashara wa Tanzania, Billnass, amesimulia kisa kilichomfanya kuacha kuamini masuala ya uganga baada ya kukamatwa na polisi muda mfupi tu baada ya kutembelea mganga.

Akisimulia tukio hilo, Billnass alisema wakati alikuwa akijihusisha na biashara ya kuuza simu mitaani, alikuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi, hata katika mazingira ambayo wafanyabiashara wenzake walipokamatwa, yeye pia hangekosa kuhusishwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema rafiki yake mmoja alimshauri waende kwa mganga ili kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

Billnass alikubali ushauri huo na kwenda kwa mganga, akiamini kwamba huenda hatua hiyo ingemsaidia kuepuka kukamatwa tena.

Hata hivyo, mambo hayakwenda kama alivyotarajia. Alisema alipokuwa akitoka kwa mganga, alianza kumweleza rafiki yake jinsi alikuwa amejipanga kuhakikisha hakamatwi tena, lakini wakati wakiendelea na mazungumzo hayo, polisi walifika na kumkamata tena.

Tukio hilo, kwa mujibu wa msanii huyo, lilimfanya kubadili mtazamo wake kuhusu uganga na kuacha kuamini kuwa unaweza kumsaidia kuepuka matatizo aliyokuwa akikabiliana nayo.

Simulizi hiyo inaangazia sehemu ya maisha ya Billnass kabla ya kujijengea jina katika tasnia ya muziki na biashara ya simu nchini Tanzania.

Share This Article