Esther Arunga arejelea jina lake la awali

Tangazo la gazeti rasmi la serikali linaelekeza arejelewe kama Esther Adongo Arunga.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa zamani wa televisheni nchini Kenya Esther Arunga, amerejelea jina lake la awali, kwa mujibu wa chapisho la kisheria kwenye gazeti rasmi la serikali.

Mrembo huyo ameacha rasmi kutumia jina la ukoo la Timberlake ambaye alikuwa mume wake na kurejelea jina lake la awali, Esther Adongo Arunga, kulingana na chapisho hilo la Oktoba 9, 2026.

Mabadiliko hayo yalirasimishwa kupitia hati ya kisheria ya kubadilisha jina iliyotiwa saini Oktoba 2, 2026, na kusajiliwa jijini Nairobi na mawakili wake wa kampuni ya LAK Advocates.

Tangazo hilo linaelekeza kwamba kuanzia sasa, anapaswa kujulikana, kuitwa na kutambulishwa kwa jina lake la awali pekee.

Uamuzi huo unahitimisha kipindi cha miaka 16 ambacho amekuwa akitumia jina la Timberlake, alilolichukua Machi 2010 baada ya kufunga ndoa na Quincy Timberlake.

Ndoa yao iliambatana na kuondoka kwake katika taaluma ya utangazaji, ambapo alikuwa amejipatia umaarufu kupitia vituo vya KTN na Capital FM. Wakati huo, pia alihusishwa na kanisa lenye utata la Finger of God.

Baadaye, wanandoa hao walihamia Australia, ambako walikumbwa na kesi nzito kufuatia kifo cha mwanao wa miaka mitatu, Sinclair, mwaka 2014.

Arunga alihukumiwa mwaka 2019 kifungo cha nje ya gereza kwa kosa la kuwa mshirika katika kosa la kuua bila kukusudia. Mumewe, Quincy Timberlake, alihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela Septemba 2023.

Share This Article