Bara Afrika linataka juhudi za pamoja zitekelezwe ulimwenguni katika kukusanya mapato ya kugharamia maendeleo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Haya ni kulingana na tamko la pamoja la viongozi wa bara Afrika lililotolewa mwishoni mwa kongamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika jumba la KICC jijini Nairobi.
Viongozi wa bara hili wametoa changamoto kwa jamii ya kimataifa kutekeleza ahadi zao kulingana na mapatano ya ufadhili ulimwenguni kutokana na kongamano la Paris. Mapatano hayo yanaamrisha kwamba hakuna nchi ulimwenguni inafaa kujipata ikichagua kati ya maazimio yake ya kimaendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakiongozwa na Rais William Ruto na mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika Moussa Faki, viongozi hao waliwasihi washirika wa kimaendeleo kuwianisha raslimali zao za kiufundi na kifedha na kuimarisha matumizi endelevu ya raslimali asili za bara Afrika.
Tamko la pamoja la viongozi wa bara Afrika lilitolewa Jumatano Septemba 6, katika jumba la KICC jijini Nairobi katika kongamano la bara Afrika kuhusu tabianchi na linafahamika kama “Tamko la Nairobi la viongozi wa bara Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi” au “The African Leaders Nairobi Declaration on Climate Change”.
Jamii ya kimataifa imetakiwa kuchukua hatua za haraka kupunguza utoaji wa gesi, kutekeleza majukumu yao, kutekeleza ahadi za awali na kusaidia bara hili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Marais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Julius Maada Bio wa Sierra Leone, Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, Ismaïl Omar Guelleh wa Djibouti, Isaias Afwerki wa Eritrea na Idriss Deby wa Chad pamoja na waziri mkuu wa DR Congo Sama Lukonde Kyenge walikuwepo wakati wa kutoa tamko hilo.
Wengine ni mkewe Rais Bi. Rachel Ruto, Naibu Rais Rigathi Gachagua, waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi, Naibu Rais wa Angola Esperança da Costa, mwenzake wa Namibia Nangolo Mbumba, katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland, aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo na mawaziri wapatao 66 kutoka nchi mbali mbali.
Rais William Ruto ametaja kongamano hilo la kwanza kabisa kuhusu mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kuwa lililofanikiwa ikitizamiwa kujitolea kwa serikali za nchi fulani, sekta ya kibinafsi, benki na wahisani kujitolea kuchanga dola bilioni 23 kwa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira kote Barani Afrika.
Kongamano hilo lilianza Jumatatu Septemba 4 na kukamilika leo Jumatano Septemba 6 katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi. Kabla ya kuanza rasmi, vijana wa bara Afrika waliandaa mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika ukumbi huo huo.