Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu, almaarufu Baba Yao, ataendelea kuzuiliwa hadi Machi 18 mwaka huu akisubiri uamuzi wa mahakama juu ya rufaa aliyokata kupinga kifungo cha miaka 12 alichohukumiwa jela.
Waititu kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Industrial Area jijini Nairobi.
Alikuwa amekata rufaa katika Mahakama Kuu dhidi ya kifungo hicho kilichotolewa na Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi Thomas Nzioki.
Nzioki alisema Waititu anaweza akakwepa kifungo hicho ikiwa atalipa faini ya shilingi milioni 53.5.
Hata hivyo, katika kumnyima dhamana, Jaji wa Mahakama Kuu Lucy Njuguna alisema haki ya kupatiwa dhamana baada ya kuhukumiwa siyo haki ya kikatiba.
Hii ni kwa sababu mfungwa hachukuliwi tena kama mtu asiyekuwa na hatia.
Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ilimhukumu Waititu kifungo cha miaka 12 jela baada ya kupatikana na hatia katika sakata ya utoaji zabuni ya shilingi milioni 588.
Waititu, ambaye alipatikana na hatia Februari 13, alihukumiwa kwa kutoa kandarasi ya kukarabati barabara kaunti ya Kiambu katika mwaka wa kifedha wa 2017-2018 bila kufuata taratibu za kisheria.
Mahakama hiyo pia ilimzuia Waititu kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa muda wa miaka 10.
Washtakiwa wenzake, akiwemo mkewe Susan Wangari, pia walihukumiwa, huku Wangari akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Testimony Enterprises Charles Chege, alitozwa faini ya shilingi milioni 295, huku mhandisi wa barabara Lucas Wahinya akitozwa faini ya shilingi milioni 21.