Serikali imeonyesha dhamira ya kuhakikisha mpango wa upatikanaji wa afya kwa wote, UHC unafua dafu nchini.
Mpango huo umetengewa shilingi bilioni 4.2 kati ya shilingi bilioni 127 ilizotengewa sekta ya afya katika bajeti ya mwaka 2024/25.
Akizungumza wakati akisoma bajeti hiyo katika bunge la taifa leo Alhamisi, Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u alisema kati ya shilingi hizo ilizotengewa wizara, shilingi bilioni 2 zitatumiwa kutoa huduma za afya ya uzazi bila malipo, bilioni zitatumiwa kwa huduma za usimamizi wa vifaa, na shilingi milioni 861.5 kutumiwa kutoa matibabu kwa mayatima, wazee na watu wenye ulemavu katika jamii.
Jumla ya shilingi bilioni 4.6 zitatumiwa kwa malipo ya wahudumu wa afya ya jamii na vilevile kuwanunulia vifaa tiba maalum vya kufanyia kazi.
Na huku ugonjwa wa saratani ukiendelea kuwa suala sugu linalowaelemea wengi, hospitali ya rufaa ya Kenyatta na ile ya Kisii Level 5 zimetengewa shilingi bilioni 1.1 zinazokusudia kuimarisha vita dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, shilingi bilioni 29.7 zimetengewa hospitali ya KNH na ile mafunzo na rufaa ya Moi ili kuboresha utoaji huduma kwa umma.