Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ametoa wito kwa asasi za usalama kufanya uchunguza wa kina na kubaini wanaohusika katika visa vya utekaji nyara wa Wakenya ambao baadaye wanapatikana wakiwa wameuawa.
Amelalamika kuwa hulka hiyo inaliharibia sifa taifa la Kenya.
Wetang’ula hususan amewataka Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Douglas Kanja, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Amin Mohamed na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kuwajibika kwa kufanya uchunguzi madhubuti kwa lengo la kuwachukulia wahusika hatua kali.
“Serikali ya Kenya Kwanza iliahidi kuzingatia na kuheshimu haki za binadamu,” alisema Wetang’ula.
“Kwa hivyo IG, DCI na DPP ambaye ni kijana wetu kutoka hapa Kakamega lazima mfanye uchunguzi wa kina na kwa haraka iwezekanavyo ili tukomeshe haya mambo ambayo yanaleta jina mbaya kwa nchi yetu.”
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi pamoja na Seneta wa Makueni Dan Maanzo wametoa wito wa kubuniwa kwa tume ya uchunguzi ili kubaini ukweli wa ni nani anayetekeleza visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela nchini.
Kanja amekanusha kuhusika kwa maafisa wa polisi katika utekaji huo wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la visa hivyo nchini katika siku za hivi karibuni.
Jana Alhamisi, miili ya wawili kati ya wanaume wanne waliotekwa katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos mwezi Disemba mwaka jana ilipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nairobi.
Hatima ya wanaume wengine wawili bado haijulikani.
Miito imekuwa ikiongezeka kwa serikali ya Kenya Kwanza kuingilia kati na kukomesha visa vya utekaji nyara ambavyo vimeziacha familia za waathiriwa zikiwa zimefadhaika.