Muungano wa Azimio sasa unataka waliomuua Rex Masai wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 jana Alhamisi wakamatwe na kushtakiwa.
Watu wengine wengi walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo.
Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi, IPOA inachunguza madai kuwa Masai alifyatuliwa risasi na kuuawa na polisi wakati wa maandamano ya jana Alhamisi.
Aidha inachunguza hali walimojeruhiwa waandamanaji wengine wanaoendelea kupokea matibabu.
Wakiwahutubia wanahabari leo Ijumaa, viongozi wa Azimio walilalamikia mauaji ya Masai wakiwatuhumu polisi kwa ukiukaji wa Kifungu 47 cha Katiba.
“Rex aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Hiki ni kisa cha kuhuzunisha chenye madhara makubwa. Tunasimama na Rex, familia yake, na waandamanaji wenzake,” alisema Kalonzo.
“Tunataka watekelezaji wa ukatili huu wa polisi wakamatwe na kushtakiwa mahakamani kwa mauaji.”
Kadhalika, viongozi hao wamewataka Inspekta Mkuu wa Polisi Japet Koome na Kamanda wa Kanda ya Nairobi Adamson Bungei kujiuzulu mara moja kwa kushindwa kutoa ulinzi kwa waandamanaji waliodumisha amani.
IPOA inasema upasuaji wa mwili wa Masai utafanyika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City Mortuary leo Ijumaa kubaini chanzo cha kifo chake.