Viongozi mbalimbali wamwomboleza Raila

Martin Mwanje
3 Min Read
Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga aliyefariki wakati akipokea matibabu nchini India

Viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanazidi kuomboleza kifo cha aliyekuwa kinara wa chama cha ODM Raila Odinga. 

Raila alithibitishwa kufariki leo Jumatano nchini India alikokuwa akipokea matibabu.

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amemtaja Raila kuwa mtu aliyekuwa sahibu wake wa kisiasa na mpatanishi ambaye daima atamkumbuka.

“Kwangu, Raila alikuwa zaidi ya mwenzangu wa kisiasa, alikuwa sehemu ya safari yangu mwenyewe katika utumishi wa umma na maishani,” alisema Uhuru.

“Nimempoteza rafiki na ndugu. Nitakosa sana mazungumzo yetu ambayo wakati mwingine yalikuwa yenye kutoa changamoto, yenye umaizi na moto wa imani ambayo daima haikuondoka machoni pake.”

Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata pia amemwomboleza kinara huyo wa ODM na kutaka urithi wake kuendelea kulitia moyo na kuliongoza taifa siku zijazo.

Nje ya Kenya, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ni miongoni mwa waliotuma ujumbe wa kumwomboleza Raila.

“Nimehuzunishwa mno na kifo cha rafiki yangu wa dhati na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. Alikuwa kiongozi mahiri na rafiki mkubwa wa India,” alisema Modi kwenye taarifa.

“Nilikuwa na fursa ya kumfahamu kwa karibu tangu enzi yangu kama Waziri Mkuu wa Gujarat na urafiki wetu kuendelea kwa miaka mingi…Natuma rambirambi kwa familia yake, marafiki na Wakenya wakati huu wa majonzi.”

Umoja wa Afrika, AU pia umeelezea kusikitishwa na kifo cha Raila na kutuma risala za rambirambi kwa familia ya marehemu na Wakenya kwa jumla.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC Mahmoud Ali Youssouf  kwenye taarifa alisema Raila atakumbukwa kama kiongozi shupavu.

“Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa kiongozi shupavu katika maisha ya siasa ya Kenya na mpiganiaji imara wa demokrasia, uongozi bora na maendeleo yanayotoa kipaumbele kwa watu,” alisema Youssouf aliyembwaga Raila kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa AUC.

“Kujitolea kwake kwa miongo kadhaa kupigania haki, mfumo wa vyama vingi na mageuzi ya kidemokrasia kuliacha alama isiyoweza kufutika siyo tu nchini Kenya bali barani Afrika.”

Rais wa Tanzania Samia Suluhu pia hakuachwa nyuma katika kumwomboleza Raila.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” alisema Rais Suluhu.

“Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote. Kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto, Mama Ida Odinga, watoto, familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Kenya kwa msiba huu. Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki, na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi.”

Viongozi wengine waliomwomboleza Raila ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed,

Website |  + posts
Share This Article