Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kupitia kwa mwenyekiti wake Wycliffe Oparanya umesema kwamba utaandikia maafisa wa polisi waraka wa kuwafahamisha kuhusu mikutano ambayo wanapanga kuandaa Ijumaa.
Mkutano mkuu utaandaliwa katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi na utaongozwa na kiongozi wa muungano huo Raila Odinga huku mikutano mingine midogo ikiandaliwa kwenye miji kadhaa humu nchini.
Kulingana na muungano huo, watakuwa wanazindua kile wanachokitaja kuwa ukombozi wa tatu.
Hitaji la sheria ni kwamba maafisa wa polisi wafahamishwe kuhusu mikutano au maandamano kabla ya siku ya kuandaliwa ili waweze kuwapa ulinzi wahusika.
Asili ya siku ya saba saba ni Julai, 7 1990, wakati viongozi tajika wa upinzani wakati huo, ambao walikuwa wakipinga uongozi wa Rais wa wakati huo Daniel Moi, waliandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa Kamukunji.
Viongozi kadhaa walikamatwa kabla ya siku hiyo na maandamano ya wananchi yakashuhudiwa katika sehemu kadhaa nchini.
Watu kadhaa waliaga dunia katika makabiliano na maafisa wa polisi huku wengine wapatao elfu 5 wakipata majeraha.
Sasa, kiongozi wa upinzani Raila Odinga ameandaa mkutano Ijumaa kama kumbukumbu ya matukio ya siku hiyo.
Ameomba wafuasi wake wajitokeze kwa wingi kwenye sehemu kadhaa ambako mikutano itaandaliwa siku hiyo kuonyesha kutoridhika kwao na uongozi wa sasa wa Rais William Ruto.
Oparanya alisema wataandika barua kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome kwa sababu wanapanga mikutano katika sehemu mbali mbali za nchi.