Askofu Sapit: Gen Z wasitishe maandamano kwa sasa

Martin Mwanje
2 Min Read

Vijana wa Gen Z wametakiwa kusitisha maandamano kwa sasa na kuipatia serikali muda wa kutekeleza mabadiliko wanayoshinikiza nchini. 

Serikali kwa upande wake imetakiwa kuhakikisha inatekeleza mabadiliko yote ambayo imewaahidi Wakenya.

Akiwahutubia wanahabari leo Ijumaa, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiangilikana nchini, ACK Jackson Ole Sapit ameonya kuwa ingawa wanaunga mkono mabadiliko yanayoshinikizwa na vijana, hawapaswi kujiingiza katika vitendo ambavyo vitahatarisha mustakabali wa taifa.

“Ingawa tunatambua Gen Z na kupongeza shinikizo zao, tunatoa wito kwao kuipatia serikali muda na fursa ya kutekeleza mabadiliko wanayoshinikiza,” alisema Askofu Sapit wakati akiwahutubia wanahabari katika kanisa la All Saints Cathedral.

“Tafadhali epukaneni na vitendo ambavyo vitahatarisha mustakabali ambao sote tunapigania.”

Askofu Sapit pia amelaani vikali kushambuliwa kwa wanahabari ambako kmeshuhudiwa nchini katika siku za hivi karibuni akisema hakuna mwanahabari yeyote anayepaswa kushambuliwa wakati akiwataarifu Wakenya.

Matamshi yake yanawadia wakati ambapo wanahabari kadhaa wanauguza majeraha baada ya kushambuliwa wakati wa maandamano Jumanne wiki hii, akiwemo Catherine Wanjeri aliyepigwa risasi za mpira mjini Nakuru.

Wadau katika vyombo vya habari wamelalamikia vikali mashambulizi dhidi ya wanahabari na kuitaka serikali kutoa ulinzi wa kutosha kwa wanahabari hao kufanya kazi zao, wito ambao serikali imeitikia.

Wakati huohuo, Askofu Sapit ametoa wito kwa serikali kufutilia mbali kodi ya nyumba na ile ya mafuta akisema Wakenya hawajaona manufaa ya kodi hizo.

Kama kanisa, ameahidi kwamba watafuatilia kwa karibu hali ya mambo nchini na kutoa ushauri wa kinachopaswa kufanywa mara kwa mara.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *