Wanafunzi 162 wa kilimo kushiriki mpango wa uanagenzi Ughaibuni

Tom Mathinji
2 Min Read
Wanafunzi 192 wa Kilimo kushiriki mpango wa uanagenzi Uingereza na Uskoti.

Wizara ya Kilimo imewahimiza wanafunzi 162 wa Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo Nchini (KSA) wanaoelekea Uingereza na Uskoti kwa mpango wa uanagenzi, kuwa mabalozi wema wa taifa.

Vijana hao wanaoelekea ughaibuni kunoa makali yao katika kilimo, aidha walihimizwa kuwa wajasiri, wakakamavu na watumie vyema fursa ibuka ili kuboresha taaluma na maisha yao.

Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alisema kuwa kilimo kinabadilika kila kuchao na kuwa cha kiteknolojia, na hivyo ipo haja ya kuwapa vijana mafunzo ya kiteknolojia katika viwango vyote vya kilimo.

Kupitia kwa taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Msimamizi Mkuu wa wizara hiyo Harun Khator wakati wa sherehe ya kuwaaga wanafunzi hao iliyoandaliwa katika Makao Makuu ya wizara ya Kilimo Jijini Nairobi, Dkt. Rono alisema ili kuboresha maarifa na utaalam katika kilimo, serikali imewekeza pakubwa katika kuimarisha uwezo wa Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo pamoja na mabewa ya Tasisi hizo kote nchini.

Wanafunzi 162 wa Taasisi ya Kilimo Nchini wanaoelekea Uingereza na Uskoti kwa mpango wa uanagenzi.

“Uwekezaji huu unatarajiwa kupiga jeki utoaji mafunzo na ukuzaji ushindani miongoni mwa vijana katika nyanja zote za kilimo,” alisema Dkt. Ronoh.

“Mpango huu unafungua fursa za kimataifa kwa vijana huku ukiimarisha ushirikiano wa kilimo kati ya Kenya na nchi za kigeni,” aliongeza katibu huyo.

Vijana hao watakuwa katika mataifa ya Uingereza na Uskoti kwa muda wa miezi sita, ambako watafanya kazi huku wakiendeleza masomo chini ya mpango huo.

Ikiwa sehemu ya nguzo muhimu katika serikali ya Kenya Kwanza, vijana 392 wamenufaika na mpango huu tangu mwaka 2023, kwa kupata ujuzi wa kilimo, ajira, ubadilishanaji wa teknolojia na kilimo biashara endelevu.

Website |  + posts
Share This Article