Mwaniaji urais nchini Ecuador Fernando Villavicencio aliuawa na watu wasiojulikana Agosti 9, 2023. Watu hao walimvamia punde baada ya kuhutubia mkutano wa kisiasa katika mji mkuu wa nchi hiyo Quito.
Alipigwa risasi mara tatu kichwani na umati uliokuwa umejitokeza kwa mkutano wake ukarushiwa guruneti lakini haikulipuka. Kifo chake kilijiri siku 11 pekee kabla ya uchaguzi.
Mmoja wa wavamizi hao anasemekana kuawa papo hapo huku wengine wakijeruhiwa.
Wiki moja kabla ya kuuawa Fernando alikuwa amemlaumu Adolfo ‘Fito’ Macias kwa kumtishia yeye pamoja na kundi lake la kampeni. Aliambia wanahabari kwamba mjumbe wa Fito aliwasiliana naye, akamwonya kwamba iwapo hangekoma kutaja kundi lao la Los Choneros, wangemvunja.
Fito ambaye ni kiongozi wa genge moja sugu alihamishwa na maafisa wa polisi kutoka jela ndogo yenye uwezo wa kusheheni wafungwa 150 na isiyo na ulinzi mkali katika mji wa bandari wa Guayaquil, hadi jela kuu iliyo na ulinzi wa hali ya juu.
Wanajeshi wapatao 4,000 na maafisa wa polisi walihusika kwenye uhamisho huo uliotekelezwa Jumamosi Alfajiri.
Macias ambaye anahudumia kifungo cha miaka 34 gerezani kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya, uhalifu wa kupangwa na mauaji ndiye kiongozi wa genge liitwalo “Los Choneros”.
Rais Guillermo Lasso alielezea kupitia mtandao wa X kwamba uhamisho wa Macias unadhamiriwa kuhakikishia wafungwa na wananchi usalama.