Wanamuziki nguli wa Tanzania Ali Saleh Kiba maarufu kama Ali Kiba au King Kiba na Juma Jux wamemwomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, aliyefariki leo asubuhi.
“Nimehuzunika sana kufahamu kuhusu kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga – Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya.” Alianza ujumbe wake kwa maneno hayo Kiba.
Nyota huyo wa muziki wa Bongo fleva alisema kwamba ujumbe wake ni kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya wote wanaomtambua Odinga huku akiitakia familia yake faraja wakati huu mgumu.
Kiba alisisitiza kuhusu huzuni aliyonayo akiahidi kusimama na watu wa familia ya Raila Odinga akisema, “Ninawaombeampate nguvu katika upendo wa wale ambao wako karibi nanyi na faraja katika urithi na kumbukumbu za mpendwa wenu.”
Msanii huyo alikiri kwamba ustahimilivu wa Raila umekuwa motisha kwa wengi nchini na hata nje na anaamini utawapa mwelekeo wapendwa wake.
Jux kwa upande wake alichapisha video ya wakati alikutana na Raila kwenye hafla moja nchini Kenya na kuandika, “Nimevunjika moyo baada ya kusikia kuhusu kifo cha Mheshimiwa Raila Odinga, shujaa wa kweli wa Afrika”.
Aliendelea kumsifia mwendazake akimtaja kuwa kielelezo cha uongozi bora, ujasiri na Umoja.
Juma alisimulia kuhusu alivyokutana na marehemu Raila na familia yake hapa Nairobi wiki chache zilizopita na anasema alijionea unyenyekevu uliofungwa na ukuu.
Naye alitoa salamu za pole kwa Rais wa Kenya William Ruto, mkewe Raila, wanawe, jamii nzima na watu wa taifa la Kenya.