Tanzania yasema haijui walipo raia wake wawili nchini Israel

Tom Mathinji
1 Min Read
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas.

Balozi wa Tanzania nchini Israel  Alex Kallua,  amesema kuwa bado hawajui walipo wanafunzi wawili kutoka Tanzania ambao walipoteza mawasiliano nao tangu nchi hiyo iliposhambuliwa na kundi la Hamas mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Sisi kama ubalozi tumetumia kila namna tunavyoweza kutafuta ukweli wa hawa ndugu zetu (wanafunzi wawili wa kitanzania walipo Israel kimasomo). Wako wapi au nini kimetokea hivyo tutakapopata taarifa sahihi tutazitoa,“ amesema Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua.

Kauli Kallua, inakuja siku kadhaa za sintofahamu kuhusu raia wawili wa nchi hiyo ambao wanaishi eneo la kusini ambalo Jumamosi iliyopita lilishuhudia mapambano baina ya wanamgambo wa wa Kipalestina wa Hamas pamoja na jeshi la Israeli.

Balozi Kallua alisema kuwa wanaendelea kufuatilia hali ilivyo katika maeneo mbalimbali na kuhakikisha watanzania wote wako salama ikiwemo kubaini walipo raia hao wawili.

“Hatuwezi kutoa taarifa za kukisia na tunaendelea kufuatilia kwa mamlaka za Israel ili kupata taarifa sahihi…

“…sisi tuko hapa ‘on the ground‘ tunafuatilia watanzania wote waliopo hapa, kuhakikisha usalama wao,“ alisema balozi huyo.

Jumatatu wiki hii, ubalozi wa Tanzania ulieleza hauna mawasiliano na wanafunzi hao wawili, wanaosoma masomo ya kilimo nchini humo huku ikibainisha kuwa ina mawasiliano na wanafunzi wengine zaidi ya 260 waliopo nchini humo.

TAGGED:
Share This Article