Mahakama Kuu ya Mombasa imempata mhubiri anayekumbwa na utata Paul Mackenzie, na hatia ya kuua bila kukusudia, kuhusiana na vifo vya wafuasi wake kwenye msitu wa Shakahola, kaunti ya Kilifi.
Akitoa uamuzi wake siku ya Ijumaa, Jaji wa Mahakama Kuu ya Mombasa Alex Ithuku alimpata Mackenzie kiongozi wa Kanisa la Good News International, pamoja na washtakiwa wenzake 18 na hatia ya makosa ya kuua bila kukusudia yanayohusiana na vifo 123 katika mkasa wa Shakahola.
Mahakama hiyo pia iliwapata washtakiwa wengine 10 na hatia ya mauaji bila kukusudia ya watu 104. Miongoni mwao mkewe Mackenzie, Rhoda Mumbua Maweu.
Mahakama ilibaini kuwa Mackenzie aliwaelekeza wafuasi kujinyima chakula hadi kufa, kupanga utaratibu wa vifo, na kuwahamishia kwenye maeneo ya kufunga, ambapo watoto walitakiwa kuwa wa kwanza, wakifuatiwa na wanawake halafu wanaume, huku Mackenzie mwenyewe akitarajiwa kuwa wa mwisho.
Hata hivyo mahakama iliwaondolea mashtaka washukiwa 60.
Mackenzie tayari alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 200 gerezani, baada ya kupatikana na hatia katika kesi nyingine ya mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190.